KENYA YANGU NAIENZI


1. Nipo hapa kung’amua, yalojaa kilindini,
Moyo unafurahia, nilotendwa nchini,
Kwa kweli kuendelea, kiuchumi nawambeni
Bahari kuogelea, ufanisi na imani,
Naienzi Kenya yangu, mithili mboni ya jicho.


2. Viongozi wana ari, wajizatiti waama,
Mambo yamekuwa shwari, ni bashasha ninasema,
Kufaulu sio siri, vitu vyote ndio vyema,
Maendeleo makini, itazidi tuwe wima,
Naienzi Kenya yangu, mithili mboni ya jocho.


3. Wananchi ni walo heri, wenye ari madhubuti,
Wao hawanna kiburi, wazalendo na wa dhati,
Tuko sisi kwa bahari, nawaelezea sisiti,
Ni chungu kama shubiri, ukuwe mtu asiyeti,
Naienzi Kenya yangu, mithili mboni ya jicho.

4. Jalia namshukuru, shaka katuondolea,
Kenya yetu iko huru, fanaka nawelezea,
Change moto metuzuru, kulihali nawambia,
Na vitu vyote mshururu, mola ametukikaramia,
Naienzi Kenya yangu, mithili mboni ya jicho.

5. Rais we twakuenzi, una ari bilashaka,
Kwa hakika ndiwe mpenzi, wa wananchi kwa hakika,
Kenya yangu ni kipenzi, limejawa na Baraka,
Maendeleo ya enzi, kayapata ya miaka,
Naienzi Kenya yangu, mithili mboni ya jicho. 
                                               Mugun Wycliffe

USIFE MOYO

1. Malenga nang’amua, yalo yakini maana,
Kuwa na ari nakwambia, atakuwezesha rabana,
Wengi takuchekelea, kukukejeli kweli sana,
Usife moyo mwandani, rabuka ni muauni.

2. Mwanagenzi jizatiti, masomo ni ngao yako,
Utakuwa madhubuti, ufanisi huko kwako,
Usitegemee bahati,tafuta wewe vitu vyako,
Usife moyo mwandani, rabuka ni muauni.

3. We rijali sikasiri, vumilia kwa hasara,
Bilashaka tia ari, uepuke masihara,
We usiwe na kiburi, nyenyekea kila mara,
Usife moyo mwandani, rabuka ni muauni.

4. Subira huvuta heri, itafika siku njema,
Utapata utajiri, ufanisi ninasema,
Hutarudi huko Misri, mambo yako kuwa mema,
Usife moyo mwandani, rabuka ni muauni.

5. Ulokwama kwa mapenzi, utafaulu hakika,
Utampata huyo mpenzi, ndo kisura bilashaka,
Mchumba atakuenzi, hautakuwa na shaka,
Usife moyo mwadani, rabuka ni muauni.

6. Na kilele nimefika, yameisha maandishi,
Ya hekima nimefoka, mfahamu dio muishi,
Msipate kuteseka, mfanikiwe kwa aushi,
Usife moyo mwandani, rabuka ni muauni.
                                             Mugun Wycliffe

 MANENO MAGENI
Kujikwatua- Kujipamba, kujitia uzuri
Misivimbi- Mistari iliyofanywa kwenye mapacho ya nyama na musuli
Kanchiri- sidiria
Zimesaki- Zimebana, zimezama, zimechopea
Behedani (bedani)- Kitu kinachonatanata nywele gundi, hutumika kupaka na kulazia nywele baada ya kuisha kusukwa
Kumpebejea- Kumrai, kumshawishi kwa ujanja na huku unajidharaulisha
Unaopuna- Unaosugua, unaoskwang’ua kwa kitambaa au pamba au kitu chochote laini wakati wa kupaka podari na kuiweka sawa usoni
Kutia watu mbioni- Kuwafanya watu watambe, wapiti wakimtafuta (Kwa sababu ya uzuri na ujanajike wake)
Kipusa- Pembe ndogo za kifaru, pia ni mwanamke anayetapiwa na wanaume na akishapatikana huwa si lolote si chochote.
Duwazi- Mtu aliyezungwa Kwa kufanyiwa mambo


           


 . SUBIRA HUVUTA HERI
1. Miye hapa nang’amua, yalojaa mumoyoni,
Kishaye mtafurahia, yake Mola maishani,
Ndiye miye nelezea, ushikilie imani,
Subira huvuta heri, mwandani ninakweleza.

2. Yule asovumilia, atamlaumu rabuka,
Kwa shida alopitia, ya maishani hakika,
Bahari taogelea, ya taabu bilashaka,
Subira huvuta heri, mwandani ninakweleza.

3. Mwanagenzi wewe soma, utilie maanani,
Utavuna yalo mema, faida kwako usoni,
Ya hekima ninasema, ni bayana maishani,
Subira huvuta heri, mwandani nina kweleza.

4. Na unayependa Mola, mtumikie kulihali,
Utafaulu inshala, mkimbilie akujali,
Utapata nazo hela, Mungu takupa kibali,
Subira huvuta heri, mwandani ninakweleza.

5. Unotafuta ajira, umwamini Maulana,
We usiwe na marara, takuauni Rabana,
Wewe kuwa na subira, utaelewa maana,
Subira huvuta heri, mwandani ninakweleza.

6. Japo mwisho nimefika, kadokeza ya rohoni,
Usipate kuteseka, ufaulu aushini,
Wewe usiwe na shaka, uvumilie mwandani,
Subira huvuta heri, mwandani ninakweleza. 
                                            Mugun Wycliffe

 

 MASOMO NGAO YAKO
1. Miye hapa nadokeza, yalojaa mu moyoni,
Kwa kweli hutapoteza, tafaulu maishani,
Hayapo na miujiza, ni ari nawambieni,
Masomo ni ngao yako, mwanafunzi jitahidi

2. Maulana muauni, ako nawe kulihali,
Ari yako maishani, ni muhimu marijali,
Na ajira we mwandani, utapata silo swali,
Masomo ni ngao yako, mwanafunzi jitahidi.

3. Achana na marafiki, wasoenzi kubukua,
Pia wale wanafiki, wa uzembe kukolea,
Watafute maashiki,wale walovumilia
Masomo ni ngao yako, mwanafunzi jitahidi.

4. Mavuno yako keshoye, vumilia kwa masomo,
Tafaulu baadaye, kazi nzuri ikiwemo,
Hela tele ni kishoye, utafuzu nalo somo,
Masomo ni ngao yako, mwanafunzi jitahidi.

5. Wasoenzi jitihada, za masomo ni fukara,
Ndiyo ni kama ibada, ni taabu kila mara,
Mwandani elewa mada, itakufanya imara,
Masomo ni ngao yako, mwanafunzi jitahidi.

6. Na tamati nimefika, kaeleza ya rohoni,
Hutapata kuteseka, tafaulu maishani,
Usipate na mashaka, majuto ya aushini,
Masomo ni ngao yako, mwanafunzi jitahidi.
                                           Mugun Wycliffe

 

MAELEZO YA USHAIRI
Mashairi haya mawili yametungwa kwa madhumuni kwanza kabisa subira huvuta heri
Ilitungwa ili kuwatia watu moyo watu wanapopitia changamoto na shairi la masomo ni ngao yako ilitungwa ilikuwatia wanafunzi mkazo wanafunzi masomoni.

HATIMILIKI.
Haruhusiwi kuyachapisha au kuyanakilia tungo hizi kwa njia ingine yoyote bila idhini ya mwandishi.Haki zote zimehifadhiwa hapa.

MANENO MAGENI
Jalali-Mungu, Rabuka, Mola, Maulana.
Kipusa-kimanzi, kidosho, msichana mrembo.
Tamati-Mwisho, hatima ya jambo Fulani,
Ucheshi-furaha, bashasha, uchangamfu.
Kilindini-ndani ya kitu Fulani k.m kilindini mwa moyo –ndani ya moyo.
Seni-mwandani, rafiki, sahibu.
Masihara-matatizo, shida, mashaka.
Dokeza-kunena, kusema jambo Fulani au kueleza jambo kwa upana.
Mithili-mfano wa, kama.
Pupa-fanya jambo wa uroho,, kwa ulafi.
Kumuenzi-kumpenda mtu Sana, kwa mapenzi.
Nawambeni-ufupisho wa neno nawambieni, inkisari.
Msenangu-ufupisho wa neno msichana wangu.
Mahamuma-msichana mzuri, banati.

MISAMIATI
A
Abjadi - alfabeti
Achari- Kiungo cha chakula chenye mchanganyiko wa pilipili siki, chumvi na ndimu au embe
Mchanganyiko wa pilipili siki, chumvi na ndimu au embe
Adawa- uadui, kutoelewana
Adibu- enye tabia nzuri
Ahlan wa sahlan- Kwa kuamkiana tu, vivi hivi tu
Aila- familia, jamii
Akidi- 1) ajabu akidi, ajabu kubwa sana
2) kufunga akidi; kamilisha ndoa
Akraba- Watu wanaohusiana kwa karibu ukoo
Amara- 1) shughuli au kazi kubwa
2) msaada
Andisi- Elekeza
Angema- kata tama
Arifu- -a kujua sana, -enye ujuzi
Asaa- inshalla, huenda, pengine
Ashiki- 1) Mtu anayependa kitu sana
2) Tamaa ya kiume au kike, uchu
Atua moyo- Shitua
Aula- bora zaidi, afadhali zaidi
Auni- 1) Msaada
2) Saidia
Awali mpaka akheri- Mwanzo hadi mwisho
Ayami (siku)- Siku nyingi
B
Bahaimu- Mtu mwenye tabia za ovyoovyo, mpuuzi
Bahari ya luja- fikira nzito
Baki (mtu baki)- mtu wa kando, asiyehusika
Banati- binti, msichana
Bashasha- uchangamfu, furaha
Beua- dharua
Bughudha- maneno yasiyofaa asemwayo mtu
Bugia chumvi ya-ishi sana, zeeka. Kutosha
Bukua- soma kwa bidii sana
Bunilizi- utanzu wa fasihi ambapo huhusika na kubuni mambo na visa visivyo halisi. Kv. Katika riwaya, ngano au tamthiliya


 

MAULANA MAISHA TUANGAZIE

1. Mbeleni nimesimama, kukweleza ewe MOLA,
Mambo mengi yaso mema,kanibana nina swala,
Muda mwingi nimekwama, najizatiti kwa hela,
Maulana kwa hakika, maisha tuangazie.

2. Maisha tuangazie, giza tele kafunika,
Kwa kweli nifunulie,la fanaka kwa hakika,
Hakika nisaidie, muda nimo kwa mashaka,
Maulana kwa hakika, maisha tuangazie.

3. Vijana katokomea, kwenye raha za dunia,
Pia nao kazembea, yakini wajatulia,
Mola tanisaidia, sina wa kumkimbilia,
Maulana Kwa hakika, maisha tuangazie.

4. Twakuomba roho zetu,kama Paulo na Sila,
Kweli maishani kwetu,ufanisi tutakula,
Tunayo bashasha kwetu, tuangazie ndo sala,
Maulana kwa hakika, maisha tuangazie.

5. Kwa mapana na marefu, twakuomba kwa yakini,
Mi sitokuwa na hofu,ndiye wewe wa moyoni,
Mambo yako bainifu,u mwokozo maishani,
Maulana kwa hakika, maisha tuangazie.

6. Bwana ndiye mchunga wangu, sitapungukiwa na kitu,
Niauni maishangu, nifanikiwe na kwetu,
Ninasema we mwenzangu, jalali ndiye wa hatu,
Maulana kwa hakika, maisha tuangazie.

                                

                                                     WYCLIFFE

SHUKRANI KANISOMESHA 

1. Zama hizi nadokeza, nina ucheshi rohoni,
Bilashaka ninaweza, kujikimu maishani,
Sijaweza kupoteza, kwa vyovyote aushini,
Shukrani kanisomesha, nina buraha ya mwaka,

2. Maisha yalo magumu, kayaaga kwa hakika,
Hela zikawa adimu, mkajizatiti mkisaka,
Mola kawarehemu, kawaauni ya mwaka,
Shukrani kanisomesha, wazazi wangu hakika,

3. Apandacho mwanadamu, ndicho atakachovuna,
Na yameshamiri humu, ufanisi,sana sana,
Sina shaka najikimu, nangamua kwa upana,
Shukrani kanisomesha, nawaenzi waama,

4. Nikamwomba maulana, kwa uvumba na ubani,
Mmeshayapata maana, ni baraka kiamboni,
Ndiye wa kweli Rabana, wa vitendo nawambeni,
Shukrani kanisomesha, Jalali yeye ni mweza,


5. Rabuka ndiye wa kweli, wewe kuwa na imani,
Ndo atakupa kibali, muheshimuni jamani,
Fanaka kila pahali, wewe umtii mwandani,
Shukrani kanisomesha, nelezea kwa mapana,

6. Na tamati nimefika, miye manju nayanena,
Msipatwe na wahaka, mfahamu yake bwana,
Kweli hakuna mashaka, ni ngome na ya maana,
Shukrani kanisomesha, ninawaenzi bilashaka,

MALENGA MUGUN WYCLIFFE
MWANAFUNZI MASENO UNIVERSITY.
MANENO MAGENI.
Hatu- ni inkisari na ni ufupisho wa neno hatua.
Waama- hakika ,kwa kweli,yakini.
Kiamboni- mastakimuni,nyumbani.
Mwandani- rafiki,seni,sahibu,.
Auni- saidia,aviza,
Manju- mtu anayetunga mashairi na kuimba utenzi,malenga,HATIMILIKI/COPYRIGHT
Hairuhusiwi kukinakili, kukichapisha au kukinukuu kitabu hiki au mashairi haya kwa njia
Nyingine yoyote ile bila idhini ya mwandishi.

                                   

 MAPENZI NI KIKOHOZI
1. Naamba yalo mdomoni, mahaba yalo ya kweli,
Yatakubana moyoni, penzi lako kulihali,
Ya daima aushini, hata usiwe na mali,
Mapenzi ni kikohozi , hayawezi kufichika,

2. Hayawezi kufichika, taeleza kwa mapana,
Ndo kisura wa hakika, mawazoni takubana,
Hautapata mashaka, takuwezesha Rabana,
Mapenzi ni kikohozi, hayawezi kufichika,

3. Utapanda na kushuka, mambo yataenda mrama,
Usipatwe na wahaka, eleza bila kukwama,
Siwe mzandiki wa mwaka, ungamue ulozama,
Mapenzi ni kikohozi, hayawezi kufichika,

4. Kaumu nipulikize , malenga miye nanena,
Ndiyo mupate muweze, kufahamu kwa upana,
Na mahaba msipoteze, bali mwelewe maana,
Mapenzi ni kikohozi, hayawezi kufichika,

5. Japo takuwa shubiri, ujizatiti mwandani,
Itakubidi ukiri, mahaba yalo rohoni,
Sahibu kuwa mahiri, ni vitendo na imani,
Mapenzi ni kikohozi, hayawezi kufichika,

6. Mweledi wa Kiswahili, naeleza kwa hakika,
mwenzangu wewe usali, utayashika Baraka,
Taondolewa maswali, jitahidi bilashaka,
Mapenzi ni kikohozi, hayawezi kufichika,

7. Ndo kilele nimefika, kayabwaga ya rohoni,
Miye manju sina shaka, kasema ya maishani,
Ukimpata malaika, utilie maanani,
Mapenzi ni kikohozi, hayawezi kufichika,

 NINA AKIMZAA MWANA.
1. Kadamnasi nelezea, naamba yalo mdomoni,
Kwa kweli tafurahia, kazaliwa kiamboni,
Na ucheshi kukolea, takosa shida jamani,
Nina akimzaa mwana, kuna mbwembwe na nderemo.

2. Mwana alo wa Baraka, ni kinara na mahiri,
Tafurahia ya mwaka, akimzaa wa ari,
Asokuwa na mashaka, mwenye baraste la heri,
Nina akimzaa mwana, ni bashasha wa dahari,

3. Atayavuna matamu, wa heshima maishani,
Kishaye akijikimu, atakuwa muauni,
Atajikaza kwa hamu, tafaulu duniani,
Nina akimzaa mwana, ni ucheshi nelezea,

4.Na asipomzaa mwana, kaumu kunungunika,
Kwa yakini wa maana, ni mrithi na wa Baraka,
Maombi kwake Rabana, bilashaka tateseka,
Malenga ninelezea, mwana ni mithili taji,

5. Mswahili sitasita, kuyasema yalo kweli,
Na waweza kujajuta, usipomlea rijali,
Hutapata matata, umtegemee Jalali,
Nina akimzaa mwana , ulimwengu kufurahi,

6. Yameisha maandiko, kayabwaga ya hakika,
Ama kweli mpate mshiko, myafahamu bilashaka,
Baadaye kuwa heko, kazaliwa wa fanaka,
Nina akimzaa mwana, kilindini ni furaha.

                                                    

 SIKU KUU YA PASAKA.
1. Pasaka ni ya maana, ni sherehe ya bayana,
Halaiki wayaona, wa bashasha sana sana,
Ufanisi kushehena, moyoni mwetu nanena,
Siku kuu ya pasaka ,tufahamu umuhimu,

2. Tufahamu umuhimu,Yesu wetu kateseka,
Tukiwa na darahimu, tusiweze kukereka,
Tujipatie nidhamu, tusiwe mkono birika,
Siku kuu ya pasaka, ukombozi tumepata,

3. Ukombozi tumepata, msalabani katufia,
Taondolewa matata, kwa kweli katuokoa,
Dunia hautajuta, kweli tunafurahia,
Mswahili nasisitiza , tusherehekee pasaka,

4. Malenga ninaeleza, pasaka ni ya ucheshi,
Alifufuka mwokozi, Yesu kristo nawambia,
Mambo yote kuwa wazi, katuauni Rabana,
Miye hapa nelezea, tusherekee pasaka,

5. Walopata majonzi, masihara au mashaka,
Sisi tukuwe wapenzi, pia tuwe na shufaka,
Na katika hizi enzi, mayatima wateseka,
Siku kuu ya pasaka, tufahamu umuhimu,


6. Kilele nimeshafika, kaeleza ya busara,
Ndio mpate kuyaweka, muepuke masihara,
Kwa bayana huu mwaka, nasema tuwe imara,
Siku kuu ya pasaka, ulimwengu tusherekee.

Kutoka kwa Mugun Wycliffe
Malenga wa Aushi
Mwanafunzi chuo kikuu cha Maseno ,kenya
Pepe:mugunwycliffe@gmail.com

 MANJU STADI
1. Jalali nipulikize, nina njozi ya hakika
Malenga miye niweze, ningamua bilashaka,
Sitaki niyapoteze, ruiya bora ya mwaka,
Ninayo njozi waama, niwe manju alo stadi,

2. Kiswahili nalienzi, mithili mboni ya jicho,
Miye ashiki au mpenzi, lugha hiki nipendacho,
Walobobea wa enzi,tanielekeza kwacho,
Ninayo njozi waama, niwe manju alo stadi.

3. Lugha hili la taifa, kwa yakini la maana,
Nitalikwea gorofa, ulo weledi bayana,
Hakuna moyo kukufa, ataniauni Rabana,
Ninayo njozi waama, niwe manju alo stadi.

4. Miye manju naeleza ,nitawaonya kaumu,
Ama kwa kweli naweza, kuwanufaisha humu,
Furi furi nimejaza, ntawapa wenye hamu,
ninayo njozi waama, niwe manju alo stadi.

5. Nina buraha ya mwaka, mola kanipa uwezo,
Manju miye nayaweka, rohoni na kwa mawazo,
Moyo hauna wahaka, nina kwakweli ujazo,
Ninayo njozi waama, niwe manju alo stadi.


6. Sio bure bilashi, nina ari kulihali,
Ujana kweli ni moshi, nina tungo si maswali,
Dunia kuna moshi, maono bora twajali,
Ninayo njozi waama, niwe manju alo stadi.


7. Naamba yalo mdomoni, njozi yangu kutimia,
Na ninalo mawazoni, moyo waifuraia,
Utaja hadi pomoni, tungo zangu kukolea,
Ninayo njozi waama, niwe manju alo stadi.


8. Hapa ninatamatisha, yote miye kayabwaga,
Kwa bahari ya maisha, ninatamba na si mwoga,
Rabuka ataniwezesha, na weledi ntawaiga,
Ninayo njozi waama, niwe manju alo stadi.


HAKIBA HII MWAFAKA.

1. Nipulikize neleze, yaloniswibu rohoni,

Kwa yakini ndo muweze, mfanikiwe jamani,

Darahimu msipoteze, myahifadhi nawambeni,

Malenga ninadokeza, hakiba hii mwafaka,


2. Hakiba hii mwafaka, hautapata dosari,

Takuauni hakika, mweledi pia mahiri,

Seni ondoa mashaka, kwa kweli takuwa heri,

Malenga ninadokeza, hakiba hii mwafaka,


3. Ujana kweli ni moshi, ujipange barabara,

Ndio upate kuishi, uepuke masihara,

Mithili na Yule mwashi, ajipatia mshahara,

Malenga ninadokeza , hakiba hii mwafaka,


4. Tuwe walio busara, tuweke ya baadaye,

Ndio tukuwe imara, tufue dafu keshoye,

Tutaacha ufukara, tafaulu baadaye,

Malenga ninadokeza , hakiba hii mwafaka,


5. Manju miye ninahoja, muyaweke mawazoni,

Hakiba sio vioja, ni bayana maishani,

Nataka muone haja, mpate hamu na imani,

Malenga ninadokeza, hakiba hii mwafaka,


6. Mswahili sitasita, kunga’mua ya moyoni,

Aila yako kupata, taadhima duniani,

Hautapata matata, Jalali takuauni,

Malenga ninadokeza, hakiba hii mwafaka,


7. Yameisha maandiko, kaeleza ya hekima,

Hata ukipata jiko, utajapata heshima,

Ninawapa wao heko, walojikaza daima,

Malenga ninadokeza, hakiba hii mwafaka,

TAMATI”

  KUFUNGA NIKAHA

1. Naamba yalo mdomoni, yalonibana moyoni,

 ndo mfahamu kiamboni, ya heri nawambeni,

ya falsafa mishani, taathima duniani,

 kutoka dadi na jadi, Jalali kaidhinisha.

2.Shabibi asiyeoa, walimwengu tamkejeli,

fedheha tajipatia, hata kwa hali na mali,

wandani tamchekelea, hirimu yake kwa kweli,

kufunga hiyo nikaha, itikadi ya daima.

3.Kisura asoolewa, kaumu kujisaili,

upweke yeye tajawa, wa mashaka kweli kweli,

hawezi kufurahiwa, na banati kulihali,

mswahili naisitiza,nikaha kweli mwanafaka.

4. Nikaha kweli mwafaka, utampata msaidizi,

wewe ondoa wahaka, ndivo mambo zama hizi,

utapata ya fanaka kuenda mrama huwezi,

ukiasi ukapera, halaiki kuchangamka.

5.Changamoto tumbi nzima, takubana aushi,

malenga miye nasema, wewe kuwwa na imani,

mwombe Mola wa rehema, kwa uvumba na ubani

itkadi za Afrika, nikaha ni ya heshima.

6. Mswahili natamatisha, jarida lenye hekima,

mng’amue ya maisha, maadili yalo mema,

na nimewaelimisha, kweny upweke mtahamu,

ukiasi ukapera, ulimwengu kufurahi.


7. Nikaha ina baraka, kweli utabadilika,

ruija yako ya mwaka, watoto wenye fanaka,

taabu utaepuka, wanao kuelimika,

ukishafunga nikaha, mwnandani utajikimu.

8.Chungu mithili ya shubiri,mwenzangu jizatiti,

utajapata ya heri, ninakwambia sisiti,

utafute ushauri, umlinde bora banati, 

kufunga ndoa nasema, ni hatua ya binadamu.

TAMATI”MASTAKIMU YA FAHARI

 1. Nipo hapa kuyasema, yalo hekima bayana,
 utayapata rehema, wa dahari Maulana,
Kesho yake ni heshima, chumba chako cha maana,
Mastakimu ya fahari, lazima ujizatiti.

2. Lazima ujizatiti, na fulusi uzitoe,
Wala sio kwa bahati, kwa juhudi jiokoe,
Kuyachambua sisiti, nadokeza situlie,
Mastakimu ya fahari, lazima ujizatiti.

3. Manju miye naweleza, mfahamu kwa upana,
Bilashaka mtajikaza, mjenge nyumba ya kufana,
Nyinyi mahiri mtaweza, mtegemee tu Rabana,
Mastakimu ya fahari, lazima ujizatiti.

4. Hakiba utaiweka, pia mkopo kuchukua,
Uepuke kuteseka, keshoye kufuraia,
Hautapata mashaka, fanaka kuogelea,
Mastakimu ya fahari, lazima ujizatiti.

5. Umwombe huyu Rabuka, kwa uvumba na ubani,
Miye nafahamu fika, utafika kileleni,
Wewe ondoa wahaka, utafaulu mwandani,
Mastakimu ya fahari, lazima ujizatiti.

6. Tafuta walobobea, wa tajriba wako heri,
Dhoruba walipitia, walijikaza kwa ari,
Wengi takuchekelea, wasioelewa siri,
Mastakimu ya fahari, lazima ujizatiti.


7. Nyumba nzuri bilashaka, itakupa taadhima,
Mambo yako kwa hakika, kuwa mufti ninasema,
Na hakiba uliweka, Mola kakupa neema,
Mastakimu ya fahari, lazima ujizatiti.

8. Malenga natamatisha, nilosema ya busara,
Vipengele vya maisha , muyashike muwe imara,
Mtakuwa wa bashasha, sio hofu kila mara,
Mastakimu ya fahari,lazima ujizatiti
“TAMATI”

 KILIMO MUFTI


1. Mbele Hapa ninaamba, maneno yenye busara,
Mambo yaende sambamba, ujikaze kila mara,
Kila siku utaimba, umepuka masihara,
Kilimo mufti nasema , ndio uti wa mgongo.

2.Malenga ninadokeza , kilimo msaidizi,
Bilashaka utaweza , kufaulu zama hizi,
Wakati hutapoteza , utavumbua ujuzi,
Kilimo mufti nasema, ndio uti wa mgongo,

3. Ninayo hoja ya mwaka, wewe tilia juhudi,
Mbolea utayaweka, seni kuwa na kusudi,
Utaepuka mashaka, mwenzangu ujifanidi,
Kilimo mufti nasema , ndio uti wa mgongo,

4. Japo yapo matatizo, swahibu ujizatitit,
Uzifuate vigezo, usitegeme bahati,
Hakika una uwezo , vipengele madhubuti,
Kilimo mufti nasema, ndio uti wa mgongo,

5. Kenya yangu naienzi , kilimo kaiboresha,
Ama kweli hizi enzi , mkopo kafanikisha,
Kwa yakini ni kurunzi, imulikayo maisha,
Kilimo mufti nasema, ndio uti wa mgongo.

6. Tafuta walobobea, wanofahamu tijara,
Bahari waogelea, wameshakuwa imara,
Hakika wavumilia, wapata kwayo ajira,
Kilimo mufti nasema , ndio uti wa mgongo.

7. Ninakunja jamvi langu, nimeboronga ya kweli,
Utoe dua kwa MUNGU, nachamba miye mswahili,
Farisi wa ulimwengu, yaache mengi maswali,
Kilimo mufti nasema, ndio uti wa mgongo.


“KILELE”

                                        

 MWANA YATIMA
1.Mbeleni niko kuchamba, maneno yenye busara,
Mambo yaende sambamba, Mola hana masihara,
Bilashaka nikumwomba, kwa uvumba kila mara,
Mwana aliye yatima, wa changamoto nasema.

2.Kuyabukua vitabu, hela zinaadimika,
Asiyapate majibu, maisha yanakereka,
Matatizo yanomswibu, moyo unafadhaika,
Mwana aliye yatima, wa changamoto hakika.

3.Walimwengu nisikize, na myatilie mkazo,
Kila kitu ndo muweze, muauni wa matatizo,
Dahari na mjikaze, msijibane na mawazo,
Mwana aliye yatima, wa changamoto hakika.

4.Mswahili nadokeza ,wazazi wana hekima,
Mwanao atajikaza, kuwaheshimu waama,
Kwa kweli wao tepuza, duniani ninasema,
Mwana aliye yatima , wa changamoto hakika.

5.Ukimwi ni janga kweli, watu wengi kafariki,
Wana wanayo kibali, twawaonea shufaki,
Kwake mola tunasali, yatima apate haki,
Mwana aliye yatima , wa changamoto hakika.

6.Nakamilisha buswati, manju miye mwadilifu,
Yatima hana bahati, ni maskini na wa hofu,
Naamba hapa sisiti, kwa bayana sijisifu,
Mwana aliye yatima , wa changamoto hakika,

“TAMATI”
 USIFE MOYO
1. Malenga nang’amua, yalo yakini maana,
Kuwa na ari nakwambia, atakuwezesha rabana,
Wengi takuchekelea, kukukejeli kweli sana,
Usife moyo mwandani, rabuka ni muauni.

2. Mwanagenzi jizatiti, masomo ni ngao yako,
Utakuwa madhubuti, ufanisi huko kwako,
Usitegemee bahati,tafuta wewe vitu vyako,
Usife moyo mwandani, rabuka ni muauni.

3. We rijali sikasiri, vumilia kwa hasara,
Bilashaka tia ari, uepuke masihara,
We usiwe na kiburi, nyenyekea kila mara,
Usife moyo mwandani, rabuka ni muauni.

4. Subira huvuta heri, itafika siku njema,
Utapata utajiri, ufanisi ninasema,
Hutarudi huko misri, mambo yako kuwa mema,
Usife moyo mwandani, rabuka ni muauni.

5. Ulokwama kwa mapenzi, utafulu hakika,
Utampata huyo mpenzi, ndo kisura bilashaka,
Mchumba atakuenzi, hautakuwa na shaka,
Usife moyo mwadani, rabuka ni muauni.

6. Na kilele nimefika, yameisha maandishi,
Ya hekima nimefoka, mfahamu dio muishi,
Msipate kuteseka, mfanikiwe kwa aushi,
Usife moyo mwandani, rabuka ni muauni.

                                      

HATIMILIKI/COPYRIGHT
Hairuhusiwi na ni makosa kuyanakili, kuyachapisha mashairi haya au tungo hizi kwa njia nyingine yoyote bila idhini Kutoka kwa mwandishi .Haki zote zimeifadhiwa humu.

  HISTORIA YA MWANDISHI
Mwandishi alizaliwa mnamo mwaka wa elfu moja mia tisa na themanini na mbili Wilayani mlima Elgon ,nilianza masomo yangu katika shule ya msingi ya kapsokwony kisha nikaenda cheptikit Academy ambako nilifanya mtihani wangu wa shule ya msingi.Baada ya kumaliza mtihani nilijiunga na shule ya upili ya kakamega ,kisha kidato cha sita kule Uganda katika shule ya upili ya Tororo.
Mwandishi ni mfanyikazi katika idara ya ugatuzi na Mipango huko Tinderet katika wilaya ya Tinderet , bonde la ufa na isitoshe ni mwanafunzi katika chuo kikuu cha maseno ambako nasomea shahada la uzamili katika maswala ya uchumi(MASTERS OF ARTS IN ECONOMICS)-2012 hadi sasa
pia nina shahada la kwanza la Uchumi kutoka chuo kikuu cha makerere katika maswala ya uchumi.(Uganda).(BA ECONOMICS)-2011