UTANGULIZI
Raphael Morondo Ongeri, halmaarufu,Ustadh Msarifu Malenga wa Bara(Malenga Ongeri) ni mtunzi wa tungo za mashairi ya bahari ainati.Amebobea sana katika tamviri hii ya Fasihi Andishi.Ameanza sanaa hii mnamo mwaka 2006 akiwa shule ya msingi,darasa la saba.Tungo nyingi za mwanzo zimeimbwa kwenye vipindi vya redio na kuchapishwa kwenye majarida ya kiswahili.Aidha,ni tungo zinakaririwa na wanafunzi wa shule za upili kwenye tamasha za muziki na kuigiza.
Raphael ni mshairi anayependa umbuji wa lugha. Amekuwa mwanafunzi wa shule ya msingi ya Nyakona(2007), Shule ya Upili ya wavulana ya Nyamagwa Nyamagwa(2011) na sasa Chuo kikuu cha Egerton (Njoro) akisomea shahada ya uanasayansi wa zaraa.
Ni mwanachama mzalendo wa Chama cha kiswahili Egerton(CHAKIE).Diwani alizobuni zimo kwenye usanjari wa uchapishaji katika matbaa mbalimbali pamoja na gazeti la Taifa Leo. Kwenye misingi ya TeknoHaMa ya kisasa iliyorahisisha kuyasoma mashairi ya huyu mshairi,baadhi ya tungo utazisoma kwenye ukumbi huu.

Raphael Morondo Ongeri
Ustadh Msarifu Malenga wa Bara

KILA UTENDAYO

1.Dunia ina vituko,na matendo yalo shani,
'Mevunjwa mengi miiko, na kuasi tamaduni,
Vinasikika vicheko,sababu mengi utani,
Kila utendayo tenda, tenda kijua tijayo.

2.Ukilitenda lolote, lolote la duniani,
Utaliacha lipite, ndio ugange usoni,
Upaendapo popote, usisahau nyumbani,
Kila utendayo tenda, tenda kijua tijayo.

3.Mtumwa ni mwacha mila,daima tukumbukeni,
Haya katu si ya hila,hata y'onekane duni,
Dhukuru kuwa ni ila,ukikataa nyumbani,
Kila utendayo tenda,tenda kijua tijayo.

4.Tenda mazuri pekee, hususani yenye kidini,
Kiama tusingojee,tumwombe wetu Manani,
Utu kwetu wendelee,tusiwe na visirani,
Kila utendayo tenda,tenda kijua tijayo.

5.Tafakari  mara mbili,kabla la mdomoni,
Sababu tuna akili,isofanana punguani,
Ubongo ulo kamili,ni ule ulo razini,
Kila utendayo tenda,tenda kijua tijayo.

6.Nachagizwa mimi sana,na watu ulimwenguni,
Madhila kutendeana,bila kite kuoneni,
Waumini kukosana,ajabu watu wa dini,
Kila utendayo tenda,tenda kijua tijayo.

7.Watu tusaili mbona,tujiulize kwa nini?
Ubaya kufanyiana,tukiwa ndugu jamani,
Tujue sisi ni wana,wake Jalali Manani,
Kila utendayo tenda,tenda kijua tijayo.

8.Kila mtu ajaribu,mnitoe kwa huzuni,
Sote twajua wajibu,wenye twapaswa 'fanyeni,
Tusitaraji majibu,pasi idili tieni,
Kila utendayo tenda,tenda kijua tijayo.

9.Tenda peke ukarimu,yalo shani yaacheni,
Nafoka yalo muhimu,kwenye watu duniani,
Sababuye tulo humu,twazama udhalimuni,
Kila utendayo tenda,tenda kijua tijayo.

10.Nasihi nikihitimu,kufikia hatimani,
Haya yote na yadumu,mwenu watu akilini,
Yote mwisho no hukumu,'sipomwamini Manani,
Kila utendayo tenda, tenda kijua tijayo.

PANDA

1.Panda ni mgawanyiko, njia na tawi la mti,
Panda ingine kunako, ala muziki ainati,
Panda kuna iliyoko, kwenye uso katikati,
Panda vitawe na viko, vya huu msamiati.

2.Panda ndiyo muatiko, mbegu na miche ya miti,
Panda pia ongezeko, kwea chombo au mti,
Panda tena iliyoko, zana ya vita manati,
Panda vitawe na viko, vya huu msamiati.

KARAMU HARAMU

 1. Nashangaa binadamu,mbona haki kudhulumu?,
Naona ni uwazimu,sizizofaa karamu,
Ninasema ni haramu, tohara sizo muhimu,
Banati jando karamu,ni kitendo cha haramu.

2.Tohara kwa maghulamu,hiyo ni nzuri karamu,
Lakini iso muhimu,mabanati kuhujumu,
Ngariba nawatuhumu,wasichana kudhulumu,
Banati jando karamu,ni kitendo cha haramu.

3.Kuna swali lilo gumu,ni nani watakadamu?
Mimi ninawashutumu,hao wasio timamu,
Ni watovu wa nidhamu,sheria hawaheshimu,
Banati jando karamu,ni kitendo cha haramu.

4.Kukeketa ni ja sumu,wala si ubinadamu,
Banati kwona ugumu,pindi kuzaa jukumu,
Mwili kweli si sanamu,eti kupunguza hamu,
Banati jando karamu,ni kitendo cha haramu.

TUTHAMINI WANAWAKE

1.Wanawake kweli watu,adinasi wa maana,
Wanaendeleza utu,sababu wazaa wana,
Wanameza mrututu,shida kuvumiliana,
Tuthamini wanawake,uchangani katulea.

2.Nina ule uhakika,mimi vyema kaleleka,
Mamangu kanieleka, ulezini katukuka,
Hadi wote zangu kaka, kubaleghe tumefika,
Tuthamini wanawake,uchangani katulea.

3.Wanawake unganeni, kataa kudhulumiwa,
Haki i mahakamani, koma sasa kukaliwa,
Msipoteze imani, vibaya mwatawaliwa,
Tuthamini wanawake,uchangani katulea.

4.Nasi wanaume pia, kutawala tudhibiti,
Tusiwe tukikalia,wanawake kama viti,
Tukifuata sheria, maisha ni madhubuti,
Tuthamini wanawake,uchangani katulea.

5.Ninawapa yangu huba, wanawake nyie wote,
Ila kwao makahaba, mnaotemewa  mate,
Kutungwa mimba si miba, msiavye mwitakate,
Tuthamini wanawake,uchangani katulea.

Malenga Ongeri.


 


  TUKIKUZE KISWAHILI

1.Kotekote yaenea, lugha iliyo thabiti,
Yakoma kudidimia, sasa inakuwa mufti,
Kiswahili kinakua, mithili miche ya miti,
Tukikuze kiswahili, daima kiwe sanifu.

2.Hususani huko pwani, thaminiwa kiswahili,
Zafuatwa nyingi fani, lugha huko ndiyo mali,
Wazifuata kanuni, kukikuza kwa idili,
Tukikuze kiswahili, daima kiwe sanifu.

3.Wapenzi wa kiswahili, lugha njema isanidi,
Tugundueni ukweli, lahaja zitufaidi,
Sisi sote tukubali, twende hatua zaidi,
Tukikuze kiswahili, daima kiwe sanifu.

4.Heko kwenu mnokuza, hata vipindi redio,
Mwondoa totoro kiza,kutupea mwelekeo,
Ujuzi mwatuongeza, tuufikie upeo,
Tukikuze kiswahili, daima kiwe sanifu.

5.Lugha ya kimataifa,ni nchi nyingi yaongewa,
Kutoka bonde la ufa, hadi pwani na visiwa,
Niseme letu taifa, Kenya nzima yasifiwa,
Tukikuze kiswahili, daima kiwe sanifu.

6.Yatumiwa mashuleni, hadi baraza bungeni,
Yafanywa kwa mitihani, wataalamu 'tahini,
Sisaili haja gani, imewekwa masomoni,
Tukikuze kiswahili, daima kiwe sanifu.

7.Kiswahili ni muhimu, tusanifu kwa bidii,
Sheng' ndiyo kwetu sumu, mufti hatukiongei,
Lugha Mombasa na Lamu, tusome kwetu Kisii,
Tukikuze kiswahili, daima kiwe sanifu.

8.Nimefika nane beti, nakikuza kiswahili,
Nafika hapa tamati, shairi lenye adili,
Tuwe na nyingi nishati, kukikuza tukubali,
Tukikuze kiswahili, daima kiwe sanifu.