Kitu na boksi
Nachukua wasaa huu, kukupa kitu na boksi
Yasikie yangu makuu, yaliyomo ndani ya boksi
Ni hiari yako mkuu,sitaki kukuletea ubosi
Usitende usiseme suu, usifikiri utaumiza utosi
Weka miguu juu, fungua uone ndani ya boksi

Ni kitu kipya, hakikuguswa na mtu
Si mtumba, wala hakina kutu
Chang'ara, meremeta, chavutia kama sumaku
Hata kabla hujafungua, chanukia kama karafuu
Marashi ya Pemba, na iriki za Tukuyu
Hata kama mbali chatoka, huko Ughaibu
Sitaki  kujidai, na sio majigambo
Kuwa napata kitu na boksi, toka ng'ambo
Ila napiga mahisabati, na kufumbua mafumbo
Jinsi MOLA alivyo nibariki, kwa mengi mambo
Sio tu kiuchumi, Afya na majengo
Pia ndugu, marafiki, na jamaa wa kambo
Hunipatia zawadi, mpya kwa boksi kimtindo
Mpaka langu jipya gari, latoka chumba cha maonyesho

Yote kenda kumi, ni baraka ilioje
Kumpata mwandani, mpenzi mpendanae
Toka kwa MOLA zawadi, wako wa pekee
Lako uaridi, hauchangii na nyuki wala wapambe
Bila shaka ya virusi, gono, wala kaswende
Kama kitu na boksi, fungua uone!!
Mashairi na Subira Mapugilo


BARUA PEPE
Barua pepe, Barua pepe
Tulizana upunguze mapepe
Njoo karibu ujumbe nikupe
Karibu na mbali upepee
Milima na mabonde uvuke
Ng'ambo ya bahari ya hindi ufike

Barua peleka salamu, kwa wangu muhibu
Ukifika kamwambie, Kwamba ninapata taabu
Na yeye ndiye wangu tabibu
Mtibabu, maradhi yangu kuyatibu
Majibu yake kwangu muhimu
Dawa tosha kwa yangu matibabu

Ninashauku ya jibu, nijibu nipate tua
Mzigo mzito unaonisumbua
Mpaka kizunguzungu chanizingua
Homa kali, na nyongo kuitapika
Fanya hima barua pepe kuiandika
Kabla pumzi hazijanishuka
Mate kunikauka, na roho kukatika

Shida yangu ni kukujulia hali, rafiki
Nataka jua kama bado nimo kwenye yako akili
Mashairi na Subira Mapugilo

SABUNI YA ROHO
Wasema penzi ni sabuni ya roho
Kwangu sabuni hii yachubua roho
Napata maumivu ndani ya koo
sijui huu ndio ugonjwa wa moyo
Du hii sasa soo!

Najua si kosa lako ni la kwangu
Wivu watawala moyo wangu
Nataka uwe wangu peke yangu
Sihusudu chochote kije kati yako na yangu
Malaika mlinzi, waridi wa moyo wangu
Mashairi na Subira Mapugilo

NAHESABU BARAKA

Kama vile mwana wa shule, nahesabu 1.2.mpaka kenda
Tofauti yangu na mtoto wa shule, shule nilishakwenda
Najua hakuna mwisho wa shule, leo nahesabu kwa kupenda
Nafikiri makini huku na kule, kwa subira na bila agenda
Ingawa ulimwengu hauna simile, NAHESABU BARAKA

Dunia haina chonde, ulimwengu haunitendei fadhira
Maisha magumu ka zege, katili na yanatesa
Walisema kuwa uyaone, cha moto nakiona
Chamtoa nyoka pangoni mwake, lakini yote maisha
Ingwa ulimwengu hauna simile, NAHESABU BARAKA

Nashindwa sijui nianzaje, kuhesabu hizi baraka
Kwani vyangu vitu vyote, nilivyo navyo ni taranta
Napata vyote bure, kwa mapenzi ya MOLA
Silipii kitu chochote, Sitaweza kidhi gharama
Ingawa ulimwengu hauna simile, NAHESABU BARAKA

Kwanza shukrani tele, kwa kupewa hewa
Bila kakala wala kerere, na bila gharama 
MUNGU Muumba pekee, ndiye ajuaye inakotoka
Ingawa Bure imejaa tele, Uhai wategemea hewa
Ingawa ulimwengu hauna simile, NAHESABU BARAKA

Pili zangu nyingi akhsante, kwa kujaliwa afya malidhawa
Iliyo jengwa kwa sembe, ngangari yangu madhubuti afya
Amenijalia mwenyewe, MOLA Mwenyeenzi Muumba
Afya ya roho ya tetere, inayo tunzwa na KRISTO Masiha
Ingawa ulimwengu hauna simile, NAHESABU BARAKA

Tena shukrani pekee, kwa kujaliwa afya imara
Afya ya mlenda na sembe, ngangali haiitaji dawa
Sihitaji tabibu mpambe, simjui yeyote mganga
Mganga wangu ni yeye, Mwnye enzi MUUMBA
Ingawa ulimwengu hauna simile, NAHESABU BARAKA

Nawaza huku na kule, nawazua bahati ya busara
Busara baraka nyingine, Busara ya kujua mabaya
Na mazuri niyatekeleze, niishi kwa amani na furaha
Duniani hata milele, naweza kupata amina?
Ingawa ulimwengu hauna simile, NAHESABU BARAKA

Naendeleza zangu akhsante, mara hii ni juu ya fedha
Ingawa sina mapesa tele, pia mimi si fukara
Nadunduliza mengi mapene, mahitaji kujitosheleza
Akiba lukuki nijiwekee, wahitaji kuwasaidia
Ingawa ulimwengu hauna simile, NAHESABU BARAKA

Nimepewa familia niipende, kwani ni zawadi tosha
Familia hii inisaidie, katika safari ya maisha
Maishani nisiwe mpweke, nitokapo kuangaika
Na nyumbani niliwazike, mahangaiko niyasahau kwa muda
Ingawa ulimwengu hauna simile, NAHESABU BARAKA


Marafiki nachagua mwenyewe, MOLA anatukutanisha
Wajibu shukrani nimpe, kwa marafiki kunipa
Kama wa mvua upinde, marafiki rangi tofauti kanipa
Tofauti ya jinsia hata maumbile, miaka na hata tabia
Ingawa ulimwengu hauna simile, NAHESABU BARAKA

Shukrani kwa sherehe, na burudani tosha
Nyimbo ngoma na zeze, michezo safari na sinema
Umenibariki uwezo nicheze, mpira wa kikapu, miguu na meza
Zaidi ya yote nikuimbie, na kukusifu wewe MUUMBA
Ingawa ulimwengu hauna simile, NAHESABU BARAKA

Siwezi hesabu baraka zote, kwani nyingine sinto zitambua
Kama nyota za mbinguni kule, jaribu wewe kunihesabia
Ingawa nina matatizo mengine, siwezi tupia MUNGU lawama
Kukosa viatu nijililie, je mkosa miguu si atajinyonga?
Ingawa ulimwengu hauna simile, NAHESABU BARAKA 
Mashairi na Subira Mapugilo

Msaada wa Kamusi

Mashairi na Tarabu za pwani

 


Malenga na wapenda mashairi huu ni ukumbi wenu wa kuvumbua, na kumwaga wenu ufundi wa msahairi na tungo. Tumeambatanisha mashairi machache, kama wataka kata kiu ya mashairi au wataka mashairi yaandikwe kwa niaba yako, au una amashairi ambayo unataka dunia ione ujuzi wako, na ipate ujumbe wako, Wasiliana nasi. 
 

Home I Love