MIADARATI SI PAKA
Heshima na taadhima, hususwan kwa vijana,
Tuweke mbele heshima, maovu yamejazana,
Sote tuweni na hima, na maovu kuyakana,
Miadarati si paka, tupeaneni ujumbe,


Hakuna cha ushujaa, ushujaa wa upuzi,
Unatafuta balaa, usijifanye mjuzi,
Yote ya shari kataa, usishike ya wapuzi,
Miadarati si paka, tupeaneni ujumbe,


'adarati haitambui,kwasi wala masikini,
Kama hilo ulijui, mimi niko na yakini,
Miadarati adui, kote tuwe mankini,
Miadarati si paka, tupeaneni ujumbe,


Majuto ni mjukuu, na mwisho uja kinyume,
Na tusijisahau tu, hakuna mume wa mume,
Kwa yakini mwia huu, kweli hakuna udume,
Miadarati si paka, tupeaneni ujumbe,


Ukijifanya jasiri, utakuja jililia,
Nawaekea nadhiri, mutakuja jijutia,
Ikiwa unafikiri, watu wana jivunia,
Miadarati si paka, tupeaneni ujumbe,


Kokote uwe sikivu, uepukane na nyange
Uwe mwenye utulivu, usishikane na nyange,
Maovu yasiwe wivu,'tajipeleka mvange,
Miadarati si paka, tupeaneni ujumbe.


Swaleh Mohammed Bakuli

Diani Coast, kenya
 
SWAHIBA SAFARI NI FUPI
Dunia ni njia kuu, waja wote wapitia,
Si wema wala waovu, wote wanaitumia,
siwe mwepesi wa povu, mwisho ukaangamia,
safari yetu swahiba, kwa yakini ipo fupi,

malimau na zabibu, yote kaletewa sisi,
kujichunga ni wajibu, kongole Binti Ramisi,
swahiba wangu muhibu, achana na ubinafsi,
safari yetu swahiba, kwa yakini ipo fupi,

usukani maishani, kwetu sisi ni IDEA,
tukiulegeza kwani, haki twakosea njia,
tafakari kwa undani, sipuuzie wasia,
safari yetu swahiba, kwa yakini ipo fupi,

manani muumba vyote, kwako mola tusitiri,
tunakoenda kokote, shari isituathiri,
chozi lisitudondoke, tuwe wakustahimili,
safari yetu swahiba, kwa yakini ipo fupi,

shikamana na hekima, na uachane na ndweo,
usishindane na nina, utakosa mwelekeo,
cha muhimu ni heshima, mola awe tegemeo,
safari yetu swahiba, kwa yakini ipo fupi,

mtegemea mwezini, na juani awezani,
mtegemea juani, mwezini ni mpinzani,
safari moja jamani, muhimu weka imani,
safari yetu swahiba, kwa yakini ipo fupi
Swaleh Bakuli


 
VIPI PENZI KUWA HIVI?
Mapenzi mwana wa penzi, mbona wanitia kero,
Asili yake ni penzi, na kaletwa na upendo,
Aliekuepo enzi, sasa anipa magendo,
Vipi penzi kuwa hivi? wengi wameangamia

Siri ya ndani ya moyo, ni chungu kheri shubili,
Afadhali kibogoyo, ajui chungu ya ndimi,
Penzi unitoa choyo, mlo kwangu ka' kwinini,
Vipi penzi kuwa hivi? wengi wameangamia

Visimani hujitia, pasi na kulazimishwa,
Bila hata kujutia, vitanzi bila kuvishwa,
Hivi ujiulizia, asubui hadi kutwa,
Vipi penzi kuwa hivi? Wengi wameangamia.
Swaleh

 
DEAR GOD
dear God, dear God,
we pray to you lord,
God of the whole universe,
the one who have mercy,

the king of king,
king of everything,
almighty the merciful,
bless our nation in full,

shower blessings upon us,
guide us from those who have been curse'
make us obeying our parents infull,
so that we can enjoy this world in joyful

dear God, dear God,
watch us in and out,
with all your blessing hands without doubt,
open our avenues through out,

keep us safe like bush from the shoe,
forever we will keep on praying you,
dear God, dear God,
no one like you

By Swaleh Bakuli, 

 Diani Coast, KenyaMAEMBO KUERA SHORO SI UBAHALULI
Tungule ngongwe tunguja, napenda nyan
ya ‘shumaa
Kushinda kilala haja, sidhani naku adaa
Nimezowela kujaja, bado na sija zubaa
Maembo kuera shoro, sio mwisho wa mawazo

Gwiji gwiji wa mawazo, sikati tama’ mapema
Bado naona ni mwanzo, japo kuwa natetema
Sitishiki na vikwazo, nacheza bila kuhema
Maembo kuera shoro, sio mwisho wa mawazo

Wahama koga ni koga, hufwata ya kipumbavu
Hupenda sana kuroga, ndede na kwa wale wafu
Na mbele wao usonga, kupita mabavu bavu
Maembo kuera shoro, sio mwisho wa mawazo

Heshima ni yangu ngao, hata shoro nikiwera
Mutakesha piga bao, nahisi tu mwajikera
Na oedua uchao, naienua bendera
Maembo kuera shoro, sio mwisho wa mawazo

Chongo chongo si kipofu, najikaza niendako
Kwenda kombo sita hofu,nakazia tu kitako
Japo maisha ya gofu,si zami kuliko kwako
Maembo kuera shoro, sio mwisho wa mawazo

Maisha yakikuzidi, subira weka kwa sala
Usiwe na ukaidi, jikaze kila mahala
Sidi mpuzi gaidi, shikana tu na utala
Maembo kuera shoro, sio mwisho wa mawazo

Japo kombo minaenda,siuachi usukani
Yote sio ya kupenda, najikaza kidumbwani
Wafriti nawachenga, ‘taki kuwa punguwani
Maembo kuera shoro, sio mwisho wa mawazo

Salala bin salale, makovu nayabandua
Siwi mwepesi wa mwale,nakaza na kukwatua
Chini sikubali kamwe, nafumba na kufumbua
Maembo kuera shoro, sio mwisho wa mawazo


S. Bakuli

 CHOZI KAVU
Ukwasi ama utule, kwangu vyote vyote sawa
Ulimbwende sifikile, pwagu usije pagawa
Dunia si kaya kale, akili wazi ka’ kawa
Chozi kavu lanitoka, shavuni latiririka

Mlipuko kalipuka, ndani ya mtima wangu
Pindi nilipo mkuta, kaenda kipenzi changu
Si pigi ngumi ukuta, leo kaniacha zangu
Chozi kavu lanitoka, shavuni latiririka

Mwia kavu mewadia, moyoni nasikitika
Pakavu nimeingia, kwa jambo la uhakika
Nabaki najichukia, furaha kufilisika
Chozi kavu lanitoka, shavuni latiririka

Kwa pamoja tulicheza, kiwanjani kunichenga
Leo nimekupoteza, machozi yana nirenga
Kukutoa nita peza, moyoni umejijenga
Chozi kavu lanitoka, shavuni latiririka

Sima tukimanga nawe, matonge nakumegea
Dogo wangu kala nae, wapi umeelekea
Sio kauta si mawe, huzuni umekolea
Chozi kavu lanitoka, shavuni latiririka

Kwa kweli kifo hakina, huruma na akiagi
Si mgonjwa si mzima, wala nani akijali
Dogo kaniacha wima, nabaki kutafakari
Chozi kavu lanitoka, shavuni latiririka

Kweli mwendo ni mfupi, mwishowe hatuujui
Tuendako si Nanyuki, fahamu ka’ utambui
Kila saa na taruki, mawazo kwangu adui
Chozi kavu lanitoka, shavuni latiririka

Manani muumba vyote, katuundia dunia
Yeye katuleta sote, sikufuru kachukia
Jitayarishe popote, kwake tutamrudia
Chozi kavu lanitoka, shavuni latiririka

Namuomba wa hisani, ulale mahali pema
Na mimi katika fani, nakupa zawadi njema
Dua zote za amani, azikubali na wema
Chozi kavu lanitoka, shavuni latiririka

Swaleh Bakuli

  

MACHO MEUPE

Kwa wale waso na haya, machoni mwao un’gara

Hulka kuanza kaya, si pwani wala mabara

Nafsi kuwadanganya, kukosa hata sitara

Usitafune mabichi, mabivu juu yaoza


Usiige hayawani, shikana na falsafa

Na acheni asilani, hekima ndio yafaa

Wapi twaenda jamani, twayatafuta maafa

Usitafune mabichi, mabivu juu yaoza


Ni changa laonekana, walitia mashakani

We bado tu wang’ang’ana, yanini upunguani

Jitahidi kujikana, sije litia ta’bani

Usitafune mabichi, mabivu juu yaoza


Wanashangaza wengine, wa’ribu waliochuma

Wakiona tu uvimbe, kifuani wanavuma

Zote tamaa jinyime, na subira kujituma

Usitafune mabichi, mabivu juu yaoza


Nasisitiza kwa mno, kwa wale waaribifu

Wakatwe yote mikono, ili wawe ni nadhifu

Wasitutie sonono, tusiwapuze ka wafu

Usitafune mabichi, mabivu juu yaoza


Nawaaga kuwambia, nimefikia mwishoni

Nadhani mumesikia, hayo yalio mwanzoni

Tayari kuyafatia, akilini na moyoni

Usitafune mabichi, mabivu juu yaoza


Swaleh Bakuli


  

BORA KIONGOZI

Swalez nauzunika, simanzi kunitawala

Lini ndugu tutafika, kama twafanywa mafala

Chozi kunitiririka,sipati hata kidala

Kheri kiongozi bora, na si bora kiongozi

Wanakuza tu zogoro, dunia ni njia kuu

Nchi yetu kichochoro,wanatudhalilisha tu

Vijana wala ugoro, aliwashutui katu

Kheri kiongozi bora, na si bora kiongozi


Wakishazidi kupata, tamaa uwazidia

Kusababisha utata, huku sisi twafifia

Ahadi na kuzikata, mbali kuzitupilia

Kheri kiongozi bora, na si bora kiongozi


Kweli wema si maneno, ni maadui wa siri

Watupora yetu meno, waacha walio kiri

Utia mingi misemo, kupora zetu akili

Kheri kiongozi bora, na si bora kiongozi


Wanafiki twawaita, ahadi azitimii

Ngangari tunaikita, na nyingi sana bidii

Njiani munatupita, amutaki kututii

Kheri kiongozi bora, na si bora kiongozi


Mikono naienua, Mungu namnyooshea

Naziomba nyingi dua, visomo kuwasomea

Mabaya kuyagundua, na mwisho kuyakomea

Kheri kiongozi bora, na si bora kiongozi


Bakuli Swaleh


 

  

MAMA WA KAMBO WA PILI

Kwako ata avya muye, pindi zinapomshika

Ni wengi wamsifue, habithi mi umuita,

Afyonza kaa ujue, punguza mwana wa Bika

Mama wa kambo wa pili, utue ubahaimu


Watesa ‘paka mteke, kumpachika shilanga

Ujali wake upweke, kuchukiza na majanga

Utawa usijitweke, imani waibananga

Mama wa kambo wa pili, utue ubahaimu


Kiulafu aongoza, tadhani ndie mchuma

Ubahau waujaza, njiani wanisukuma

Sakafuni wanilaza, bila hata ya huruma

Mama wa kambo wa pili, utue ubahaimu


Matambara kwangu nguo, aibu kwako pungufu

Wasemeza kwa tutuo, imani kwako hafifu

Nakupa jina shanuo, si kuli uko nadhifu

Mama wa kambo wa pili, utue ubahaimu

Laana au uchawi, nashindwa kuvitambua

Usiyakate matawi, shinani kutaungua

Nikuze na nistawi, mzigo nita kutua

Mama wa kambo wa pili, utue ubahaimu


Swaleh Bakuli


  

HONGERA NINA

Mwenyezi Mungu jalali, shukru wasitahiki

Katoka ndani halali, salama bila ya dhiki

Usiku nina alali, na usingizi ajipi

Hongera nina mlezi,Manani akunusuru


Kitabia kanifunza, kanikataza mabaya

Yote mema kunijuza, nashukuru sikupwaya

Asante kwa kunikuza, kinyume na yote haya

Hongera nina mlezi,Manani akunusuru


Mema ukanifundisha, sambamba na ya kidini

Kujali yangu maisha, nina ni mwenye imani

Leo naweza jilisha, tena peke’ kwa yakini

Hongera nina mlezi,Manani akunusuru


Manani atakujazi, duniani na akhera

Mema ayaweke wazi, na sio ya kukukera

Nakushukuru mzazi, kwa kunipa nzuri sera

Hongera nina mlezi,Manani akunusuruSwaleh Bakuli


  

MOLA ASTAHIKI SHUKRANI

Upepo wavumavuma, ukwasi uteletele

Ndanie waja uchuma, uchumi kama upele

Katujazia Muumba, ili njaa tusilale

Manani mtakatifu,aitaji shukrani


Wasafiri watumia, juu bila ya kuzama

Ndani pia uingia, kwa uwezo wa rabana

Si jisifu kasifia, ukajitia lawama

Manani mtakatifu, aitaji shukrani


Starehe mwaendea, haya kukosa usoni

Maovu kuitendea, waja hamuoni soni?

Soma akili bobea, ujitoe utongoni

Manani mtakatifu, aitaji shukrani


Bakuli Swaleh

 

USI SHANGAE YA NSI

Eti meli kuholea, na ndege juu angani

Si shangai kuonea, sivyo vya ajabu kwani

Macho kuvikodolea,shangaa na vya Manani

Si shangae na ya nsi, wayajua ya Muumba?


Vipi mbingu kusimama, wima bila ya uguzo

Usiku ukisimama, juu tapata mvuto

Sifa nyingi zabanana, washangaa na mafuso

Si shangae na ya nsi, wayajua ya Muumba?


Ni mbali tuliko toka, tumboni miezi tisa

Nina du sivyo kasota, mtihani kaupita

Sasa waitwa Dokta, gwiji pia wajiita

Si shangae na ya nsi, wayajua ya Muumba?


S. Bakuli

 
  

SONDO MTI

Tunafaa kutafakari, kwa yote wanayo sema

Huficha zao habari, eti uovu watema

Si wote wanao Sali, ukadhani wote wema

Uzuri wa mkakasi, ndani kipande cha mti


Akunyonyae si Yule, Yule alioko kule

Hajali wako utule, na ukwasi wa kiume

Ujitia ni waume, na kujihisi wafalme

Uzuri wa mkakasi, ndani kipande cha mti


Si wema ni wenye inda, na vibweshu hutuona

Na uovu kuulinda,ili wema kuudona

Kimaisha ukipinda, upoza chao kidonda

Uzuri wa mkakasi, ndani kipande cha mti


Hukutesa kiakili, lengo tu kukumaliza

Ni kama nduma kuwili, auma na kupuliza

Chunga usijitairi, na ubaya kulipiza

Uzuri wa mkakasi, ndani kipande cha mti


Tuwache ubinafusi, hima dini kuishika

Siwe wale wafuasi, ukaja ukadhurika

Wema sio wote nsi, majina tu ujitwika

Uzuri wa mkakasi, ndani kipande cha mti


Ajitia ashauri, usiku yuko angani

Mazuri kuyaghairi, kuyapeleka pangani

Niwabaya wa kisiri, ukudhuru kwa amani

Uzuri wa mkakasi, ndani kipande cha mti


Ukingoni nafikia, sikoka wala simani

Wabaya kuwachukia, mi ni dawa ya amani

Mkono nawapungia, ujichunge na mwendani

Uzuri wa mkakasi, ndani kipande cha mti


Swaleh


  

SOKA MWITUNI

Wacheza soka mwituni, ni tamu hila hatari

Sokisi huna migu’ni, wajifanya we hodari

Siwe kama malauni, kujifurisha kidari

Wenzangu soka mwituni,ni vipi munaicheza


Sokisi hamzivai, vipi miba mwaikwepa

Musifanye sitizai, mukashindwa kunenepa

Usifanye usodai, ukafunga na kusepa

Wenzangu soka mwituni,ni vipi munaicheza


Ni asali zimejaa, mwituni mwakimbilia

Au mwafanya mzaa, popote tu mwaingia

Usije ukashangaa, mwiba ukajidungia

Wenzangu soka mwituni,ni vipi munaicheza


Pindi nyuki wakitoka, mtapata matokeo

Hakuna pakutoroka, utabaki tu pekeo

Toka kabla hujachoka, si patwe na ya kileo

Wenzangu soka mwituni,ni vipi munaicheza


Popote we mchezaji, usisahau sokisi

Lazima uihitaji, usije leta mikosi

Jivunie kama taji, mfukoni mi sikosi

Wenzangu soka mwituni,ni vipi munaicheza


Swaleh


  

PENZILE LI TAMU

Muhibu nakuthamini, usinitie majonzi

Sije danganywa na ndimi, ukanitoa machozi

Moyoni niweke mimi, mara mbili kama jozi

Madubi kipenzi changu, sikuachi asilani


Magharibi mashariki, kusini kazkazini

Wengine sibabaiki, wala kwao sita zini

Si kwa raha si kwa dhiki, sitakutoa moyoni

Madubi kipenzi changu, sikuachi asilani


Wivu kwangu sitaacha, najali kupindukia

Kukupenda nitachacha, penzi limenizidia

Sitalaumu pakacha, kwa maji kulitilia

Madubi kipenzi changu, sikuachi asilani


Sita yashika ya wale, wale walioko pale

Utamaliza karne, haunibanduki kamwe

Usishikane na nyange, muhibu wangu jichunge

Madubi kipenzi changu, sikuachi asilani


                          Bakuli Swaleh

Diani Coast, Kenya